Involvement

RUKA NAMI

{Picha kwa hisani ya birdfact}

 

Na Abdul S. Shaban

Wewe ni ndege mzuri, zavutia zako mbawa,
Harufuyo ya uturi, niumwapo ndiyo dawa,
Nuru yashinda kamari, inawaka maridhawa,
Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami.

Naomba uruke nami, ndiyo ya kwangu maombi,
Chini kuna tsunami, ina makubwa mawimbi,
Ukidondoka na mimi, kufa nawe sio dhambi,
Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami.

Ukiweza nami ruka, kiotani kuniacha,
Napenda vyako vibweka, na kelele kukikucha,
Naamini tateseka, mpweke ukiniacha
Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

Turuke wote angani, nipeleke kule juu,
Nikudekee mwandani, ka bibi na mjukuu,
Washangae insani, sitaki zao nahau,
Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

Ni radhi kuacha nyumba, kuishi kwenye kiota,
Walosema ninayumba, wazi wazi watajuta,
Walochukia uchumba, kilingeni mewakuta,
Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

Sauti ndege wengine, wazipaza kweli kweli,
Kuna za wale wanene, wenye ukubwa wa mwili,
Wakatafute pengine, sisikilizi badali,
Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

Tena vyema kunilinda, hilo la kwako jukumu,
Niliwaze kama kinda, kwa upole na nidhwamu,
Ninajua wanipenda, moyo meshika hatamu,
Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

1 thought on “RUKA NAMI”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top