Involvement

MTI ULIOPINDA

{Picha kwa hisani ya Warren Photographic}

 

Na Abdul S. Shaban

 

Hakiwezi kunyooka, kivuli cha mti huu,
Toto la nyoka ni nyoka, majuto ni mjukuu,
Maovu ukiyataka, sifanyie mji huu,
Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

Kivuli kitafuata, umbile la mti wake,
Ikiwa kitakupata, mtoto kinyesi chake,
Hutakiwi kuukata, osha mkono sinuke,
Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

Kama hivyo basi ndivyo, twapaswa kuzingatia,
Mkubwa akiwa ovyo, watoto huiga pia,
Watafata hivyo hivyo, tabia zilosalia,
Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

Kama haujatulia, wapenda kujivinjari,
Watoto huangalia, mwenendo kuukariri,
Keshokutwa wasikia, dogo kalewa chakari,
Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

Mavazi wajivalia, vimini ama vinjunga,
Wana kuwanunulia, barabarani mwatinga,
Hivyo unavyowalea, vibaya unawajenga,
Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

Hata iwashike dhiki, kunyooka musichoke,
Kivuli hakinyooki, hufata matawi yake,
Kwenye hilo tia tiki, mashaka usiyaweke,
Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

Maana nimeiweka, na mwisho ninakomea,
Kalamu imeandika, usia kuwatolea,
Munapaswa kuushika, musije kuangamia,
Kivuli hakinyooki, kama mti ukipinda.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top