Na: Dorothy Waweru
dorothywaweru161706@daystar.ac.ke
Sikukuu ya Moi chuoni Daystar ilisherehekewa kwa mbwembwe, vifijo na nderemo kwani katika uga wa “Santiago Barna Betheli” kama unavyojulikana na wacheza kandanda wengi, mchuano mkubwa ulikuwa ukiendelea. Mchuano huo uliandaliwa na wanafunzi wacheza kandanda ikiwemo; Walter Nalwa, Nicholas Atulo Snr, Cedrick na Dadiseh Olwaga ambao walinuia kujiburudisha katika mchezo huo wa miguu.
Mchuano huo ulijumuisha timu sita zikiwemo: Blueboys, Rawa, Buffoons, Bomboclats, DCF handball na Fimbu. Timu hizi zilimenyana vilivyo ili kushinda zawadi murwa ambayo ilikuwa ni mbuzi mzima. Timu za Buffoons na Rawa ndizo zilifungua uga huo ambao ulikuwa na utelezi kufuatia mvua kubwa iliyokuwa imenyesha usiku wote.
Timu ya Buffoons ilijikakamua katika dakika za kwanza huku Caleb Msando akiifungia timu hiyo bao la kwanza naye Nicholas Atulo Snr akifunga bao lao la pili. Timu ya Rawa ilijikakamua katika kipindi cha lala salama ambapo John Lemaiyan aliifungia Rawa bao lao la kwanza. Kitengo hicho cha kwanza cha mchezo kilipotamatika, Buffoons walikuwa wamefunga mabao mawili kwa moja.
Mashabiki wa timu ya Buffoons walijaa uwanjani wakiimba nyimbo za ushindi kwani timu hiyo ingemchinja mbuzi kama zawadi ya ufanisi wao iwapo wangewashinda wenzao kwenye semifinali. Baada ya dakika chache za mapumziko, timu ya DCF handball ilijitosa uwanjani kumenyana na wachezaji wa timu ya Fimbu. Uzoefu mkuu katika mpira wa mikono wa timu ya DCF handball ulionekana kuwapa mkono uwanjani. Hata hivyo baada ya dakika kumi na tano Wallace kutoka timu ya Fimbu alifunga bao la kwanza. Baada ya dakika zingine tano, DCF handball ilisawazisha kupitia mchezaji Ephantus.
Baada ya nusu wakati wa mchezo huo, timu ya Fimbu ilifunga bao lingine ambalo liliwawezesha kuibuka washindi katika kitengo hicho kwa mabao mawili kwa moja. Timu ya Blueboys vilevile ilichuana na timu ya Rawa huku wakifunga bao lao la kwanza ambalo lilikuwa la pekee katika mchezo huo hivi basi kuibuka washindi dhidi ya Rawa.
Hata ingawa jua lilikuwa mtikati, wachezaji wa Bomboclat waliingia ugani kumenyana na DCF handball. Yasemekana kuwa wachezaji wa Bomboclat walikuwa wamekesha wakijitayarisha kwa mchuano huo wa kipekee. Katika dakika za kwanza, Bomboclat ilifunga bao lao la kwanza na baadaye kufunga la pili. DCF handball ilijizolea nunge hivi basi Bomboclat kuibuka washindi.
Isitoshe, kabla ya semi fainali, Bomboclat ilichuana na Fimbu na wakailaza Fimbu bao moja kwa nunge. Timu zilizofuzu kwenye semi fainali ni Fimbu, Buffoons, Bomboclat na Blueboys. Mechi ya kwanza katika semi fainali ilikuwa kati ya Buffoons na Fimbu. Buffoons walilazwa bao moja la kufunga virago baada ya kucheza kwa ukakamavu mwingi sana.
Nyuso za wachezaji wa timu ya Buffoons zilijaa simanzi kwani mbuzi alikuwa amewakwepa. Lisilobudi hubidi, Buffoons walidondolewa kwenye mchuano wakabaki kuwa mashabiki tu. “Ni uchungu sana mama kubeba mimba tumboni kwa miezi tisa halafu anampoteza mwana wake. Nasikitika sana kuwa tumeshindwa,” Duncan Olile, kipa wa timu ya Buffoons alisema.
Timu za Bomboclat na Blueboys zilichuana kwenye mchezo wa pili katika semi fainali huku Bomboclat ikiibuka mshindi baada ya kuilaza Blueboys mabao mawili kwa nunge. Washindi wa semi fainali walikuwa Bomboclat na Fimbu. Wakati ukiwa saa kumi na mbili kamili, mchuano kati ya timu hizi mbili ulianza huku Bomboclat ikifunga mabao mawili mida ya dakika za kumi na tano za kwanza. Japo Fimbu iling’ang’ana kiudi na uvumba kujizolea angalau bao moja, jitihada zao hazikuzaa matunda kwani katika kipindi cha pili cha mchezo huo, Bomboclat ilifunga bao lingine. Bomboclat wakafunga mabao matatu kwa nunge.
Mbwembwe na shamrashamra zilijaa uwanjani wakati ambapo wachezaji wa Bomboclat walipokabidhiwa mbuzi wao. Wachezaji waliachwa ugani wakisherehekea ushindi wao huku mashabiki wakiungana nao kushangilia ushindi wao.