Involvement

  BIASHARA YA OMBAOMBA

{Picha kwa hisani ya Mwananchi}

 

Na: Gertrude Prosper

{getrude2003@gmail.com} 

Tumekua tukiona watu ikiwemo watoto na wazee walemavu barabarani wakiombaomba ili waweze kujikimu kimaisha. Ila cha kushangaza ni kwamba wengi wao wapo kibiashara, na sio tu biashara ya kawaida ila ni ile ya kutumikishwa.

Baadhi ya watu hawa wanageuza kuwa mtaji, na nyuma yao ni watu wenye uwezo wanaowatumia ili kunufaika na kufaidi hizo hela au msaada unaotolewa kwa watu hawa. Kisichoaminika ni kua pesa hizo hupitia hesabu ya hali ya juu kama tu mapato mengine. Walemavu wengi hulazimishwa kutimiza matakwa ya waajiri wao ingawa hawaipendi kazi hiyo, kwani “Lisilo budi hutendwa.” Wengine wao wanahadaiwa kua wanatajirika katika biashara hio lakini mwishowe wanateswa, kunyanyaswa na kulipwa kiasi kidogo kisichowatosha.

Changamoto inatokea pale mtu anapotaka kuwasaidia watu hawa wasiojiweza, anashindwa kujua nia ya kweli ya watu hao wanaohitaji msaada, kumbe wapo hapo kwa kulazimishwa.

Watoto walemavu pia wanalazimishwa kuomba mitaani na wasipoleta pesa hua wanapigwa. Familia nyingi zinadanganywa kuwatoa watoto wao na kuenda kufanyishwa biashara ya kikatili na haramu. Watoto hawa wanasafirishwa na kuletwa kuja kutumikishwa mbali na wazazi wao na kulamishwa kukatika mawasiliano na wao.

Kwa watoto wanaotumikishwa, imegundulika kua chanzo ni malezi. Wazazi au walezi wanadanganywa watoe watoto walemavu na kupewa ahadi kua watapewa misaada ya kifedha kama malipo yao ilhali watoto hao wanaenda kuteswa. Wazazi na walezi hawa wanatakiwa kuzingatia malezi ya watoto wao walemavu na kuhakikisha hawakati  tamaa kwa watoto hao na badala yake kuwalinda ili kuepukana na mazingira hatarishi. Jamii pia inatakiwa kuhakikisha kwamba watoto hawa walemavu wanalindwa ili wawe raia wema na sio mzigo kwa Taifa. Sio watoto tu, hata wazee walemavu wanahitaji ulinzi kwa sababu wanyanyasaji hawa wananufaika wakijua watu hawa wenye ulemavu hawajiwezi na wengine wametelekezwa.

Hata hivyo, mbali na hawa wasiojiweza kutumikishwa, kuna walemavu, wanaofanya ajira hii kwa hiari kutokana na hali yao ya maisha kua ngumu, na hio ndio njia pekee itakayowawezesha kuishi na kutunza familia zao kwa wale wenye watoto. Wamama wenye watoto walemmavu au wamama mlemavu wenye watoto na wameachwa na waume zao kutokana na hali yao, huteseka sana. Walemavu hawa wanakubali kutumiwa kama vitega uchumu ingawa ni kwa mateso, kwani kwao “heri nusu shari kuliko shari kamili”.

Hali nyingine ni ya ombaomba tapeli, ambayo pia ni biashara inayofanywa na baadhi ya watu wanaojifanya walemavu wakiombaomba ilhali si walemavu bali ni matapeli. Watu hawa wameamua kuanza biashara hii kwani wanaamini kuwa watu huwasaidia au kuwapa fedha watu wenye ulemavu tu. Mwisho wa siku, utawaona watu hawa wakielekea nyumbani bila ulemavu wowote, baada ya kuvuna ambapo hawakupanda.

Watu hawa utawaona wakitambaa barabarani wakiwa wamevaa mavazi yaliyochakaa kabisa ili watu wengine waamini kuwa hawajiwezi. Kuna baadhi yao pia hukodisha watoto wao au wa ndugu na kuwatumia kama kitega uchumu ili tu wahurumiwe na kuchangiwa pesa. Wengi wao hutumia usafiri wa bodaboda ili wasionekane au kujulikana na watu.

Biashara hizi za ombomba ni kinyume na sheria kwani inawazuia watu wenye ulemavu kutopata msaada kwasababu ya uoga uliojawa watu ya kuwa wanatapeliwa. Wapita njia wengi na hata waendesha magari wamepunguza kiasi cha kuwasaidia ombaomba barabarani kwa sababu wengi wao hawana ulemavu na hawaaminiki.

Serikali inatakiwa kuwasaidia walemavu hawa na kuwashika hao matapeli  wanaojifanya.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top