Involvement

 MFANYAKAZI WA NYUMBANI

{Picha kwa hisani ya Conde Nast Travelers}

 

Na: Gertrude Prosper

{getrude2003@gmail.com}

Kwa miaka mingi sasa watu wengi wamezoea kuwaajiri wafanyakazi wa ndani ili kuwasaidia kazi. Wafanyakazi hawa wa nyumbani ni wasaidizi au wakelezaji wa kazi zote za nyumbani ikiwemo kufua, kupika, kufanya usafi wa nyumba na mazingira, kuosha vyombo na baadhi ya kazi zingine nyingi wanazopewa na waajiri wao. Mbali na kazi hizo, wafanya kazi wengi hupewa kazi ya kulea watoto endepo mama au wazazi ameenda kazini, au kama wanataka kuendelea na shughuli zingine.

Kabla sijaelezea jinsi baadhi ya mambo ya ajabu ambayo wafanyakazi huwafanyia watoto, tutaanza na jinsi wafanyakazi hawa huteswa katika baadhi ya sehemu wanapoajiriwa. Kwanza kabisa, mtu anapomwajiri mfanya kazi anatakiwa ahakikishe kua hamtesi wala kumyanyasa kwa namna yoyote ile, na badala yake anatakiwa akumbuke haki yake. Hii ni kwasababu wafanyakazi hawa ndio walinzi wa nyumba na wana uwezo wa kuiangamiza au kuistawisha familia.

Wafanyakazi hawa hupitia changamoto nyingi kama vile kunyimwa chakula na mavazi mazuri, kupigwa, kutopewa mahali pazuri pa kulala, kufanyishwa kazi nyingi nje ya uwezo wao na hata kubakwa au kunyanyaswa kijinsia na waajiri wao. Waajiri hawa husahau mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi hawa ingawa bado wanawahitaji.

Kumetokea kesi nyingi ya wafanyakazi hawa wa ndani wa kike, kubakwa au kunyanyaswa kijinsia na waajiri wao wakiume na hii imeleta migogoro katika familia nyingi na kusababisha kuvunjika kwa ndoa. Wengi wao wakitoa malalamiko, hawaaminiwi kwa sababu wanalaumiwa kuwa sababu ya kilichowapata. Unapata mume au baba mwenye nyumba ana familia ya pili na mfanya kazi wa ndani.

Kuna baadhi ya haki ambazo wafanya kazi wanastahili kupewa ikiwemo likizo kwa sababu wengi wao hufanya kila siku bila kupumzika na inawalazimu kusingizia kuumwa ili waweze kupumzika au kuenda kuwasalimia wazazi wao nyumbani. Wanatakiwa pia walipwe mishahara yao kamili na kwa wakati, na kuhakikisha ulinzi wa afya na usalama wao.

Kati ya hayo machache kuhusu haki na usalama wa wafanya kazi wa nyumbani, tutaangazia vitendo vya ajabu vinayofanywa na wafanyakazi hawa katika familia tofauti haswa kwa watoto wanaoachiwa kuwalea.

Wafanya kazi hawa wa ndani hushikwa wakiwadhulumu, kushiriki kingono na watoto wa waajiri wao na wakati mwingine kuwapiga na kuwaumiza watoto hawa. Inasikitisha kwa sababu watoto hawa hushindwa kutoa mashtaka kwa wazazi kutokana na umri wao kua mdogo na sababu nyingine ni vitisho wanavyopewa. Wafanya kazi wengi hunyanyasa watoto kwa sababu ya kukosa subira pindi mtoto anapokataa kula, kulala au kumsikiliza.

Wazazi hawa hugundua hizi shida na mateso watoto wao wanayoyapitia baadae sana wakati mtoto ashaharibiwa kupitiliza. Kesi nyingi zimetolewa dhidi ya wafanya kazi wa nyumbani lakini bado idadi inatia shaka. Wazazi wanatakiwa wahakikishe wanawaajiri wafanyakazi wazuri waliobobea ili watoto wao wawe kwenye mikono salama, kwa sababu wakati mwingi wapo kazini na wanachelewa kurudi hivyo hawajui kinachoendelea nyumbani. Wakati mwingine wazazi hawa wanashauriwa angalau kukaa na mtoto kwa muda mwingi na sio tu kutokomea kazini ilhali mtoto hayupo salama.

Kutokana na uzoefu wa kuwaachia wafanya kazi wa nyumbani watoto ili wawalee, hamna namna nyingine bali kuhakikisha wafanya kazi hawa ni wa kuaminika na wenye utu na huruma.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top