Involvement

WAPI NJIA NITAPATA?

Na Abdul Shaban

Ndugu zangu ahlani, wasahlan jamia
Nawaombea amani, iweni nanyi daima
Nimenena kwa vinani, taarifa kuwafika
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Mwenzenu nawambieni, limenikuta gharika
Chonde chonde sikizeni, nipatapo saidika
Sitanena kwa uwazi, adui atang’amuza
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Nimo ndani ya bahari, nimezama kwa pupa
Hali imetahayari, sina hata pa kushika
Mchana hapapo tuli, usikupo kwachafuka
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Nilifanya sana siri, pale nilipompata
Nikataka msitiri, shida zake kumputa
Kumbe ndiye baladhuli, wahida hanayo sifa
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Sikufata desturi, nikajivika upapa
Sikuskiza shauri, uziwi ulinishika
Nikajivika makini, kumbe sina maarifa
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Baharini si shwari, nimeloa chapachapa
Maji chumvi kooni, yaniwasha kwa hakika
Wadudu wa baharini, nawano wanichonyota
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Nimekuwa maskini, sina hata pakushika
Kila nikipiga mbizi, maji nayo yanivuta
Sina cha kujistiri, ngiri nayo yaniliza
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Wapi ndugu majirani, waja wote wanipita
Mniswamehe jamani, nimejifunza hakika
Wavuvi na makuhani, kwa pamoya nawaita
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Msiniache jamani, mwenzenu nahangaika
Nimenena hadharani, mnipe njia kupita
Nisijepo buriani, nyote mkaumbuka
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Nimenena bila khini, ili nipate ng’amuka
Yeye kashika mpini, msijepo kwa pupa
Chukueni tahadhari, sote aso tuzamisha
Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top