Involvement

TUKICHEZA TUTAJUTA

 

Na ABDUL SHABAN

{abdoolmtyro@gmail.com}

 

Zama zimerudi tena, kwenye hali ya siasa,

Sasa hawa waungwana, watayamwaga mapesa,

Nami nawaasa sana, kutorudia makosa,

Ama tutakujajuta, kama miaka ya nyuma!

 

Wengi tulowachaguwa, tukiwadhani wakweli,

Uchumi watainuwa, ziinuke zetu hali,

Katika kila hatuwa, hatukuipata sahali,

Sasa tusije kujuta, kama miaka ya nyuma!

 

Vyama walivyovijenga, visitutie tamaa,

Heri mtu kujipanga, tukakataa hadaa,

Wametufanya wajinga, na hakuna la kufaa,

Kwayo tusitake juta, kama miaka ya nyuma!

 

Wengi wako kwa tamaa, na malengo ya binafsi,

Huku wanatuhadaa, kwamba eti wako nasi,

Vyeo wakisha vitwaa, ndio hao huwa basi,

Tusipige tukajuta, kama miaka ya nyuma!

 

Tuwatizame matendo, tusiyashike maneno,

Asofaa tupa kando, angatowa donge nono,

Huyo kaja kwa mawindo, wako wengi kwa mfano,

Tukiwapa tutajuta, kama miaka ya nyuma!

 

Kura yako usiuze, jitahidi kuwa wima,

Wakisema wasikize, huku uwe wawapima,

Wasofaa tuwapuuze, hawafai kusimama,

Au sivyo tutajuta, kama miaka ya nyuma!

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top