Involvement

Matokeo za mechi ya ligi ya mabingwa barani Ulaya

[Picha kwa hisani ya FC Barcelona]

Na Dennis Mungai

Msimu mpya wa ligi kuu ya mabingwa barani Ulaya ulianza jana usiku huku mechi nane zikichezwa. Newcastle United walianza msimu wao dhidi ya AC Milan baada ya kukosa kushiriki michuano hii kwa miaka ishirini. Mechi hiyo ilikamilika sare tasa, kila timu ikitoka na alama moja. Timu nyingine katika kundi lao, Paris St Germain waliishinda Borussia Dortmund kwa mabao mawili kwa sufuri.

Kwingineko, Barcelona waliiduwaza Royal Antwerp 5-0 huku mabingwa watetezi Manchester City wakitoka nyuma na kuilaza Crvena Zvezda mabao matatu kwa moja. Leipzig walipata ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Young Boys huku Feynoord wakipiga Celtic 2-0. Vigogo wa Ligi kuu nchini Uhispania Atlético Madrid walitoka sare ya bao moja dhidi ya Lazio nayo Porto ikashinda kwa mabao matatu kwa moja walipochuana na Shaktar Donetsk.

Michuano itaendelea leo usiku huku mechi inayosubiriwa na wengi ikiwa ni kati ya Manchester United dhidi ya Bayern Munich. Vijana wa Erik ten Hag wana masaibu baada ya kumpoteza mchezaji mwingine, Aaron Wan Bissaka, kwa jeraha na kupata kipigo cha 3-1 dhidi ya Brighton siku ya Jumamosi. Timu ya Arsenal inarudi katika michuano hii baada ya miaka saba nje. Wataanza msimu wao dhidi ya PSV ya Uholanzi.

Mabingwa mara kumi na tatu Real Madrid wataialika Union Berlin ya Ujerumani, mashabiki wa Los Blancos wakipendezwa na kutarajia mengi kutoka kwa mchezaji wao mpya Jude Bellingham. Timu iliyofika fainali msimu uliopita Inter Milan watakabiliana na Real Sociedad huku washindi wa Kombe la Europa msimu uliopita Sevilla wakiialika Lens ugani Ramon Sanchez Pizjuan.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top