Skip to content

Involvement

Home » Mama

Mama

(Picha kwa hisani ya Dreamstime.com)

{Limetungwa na Abdul Shaban}

Uzima na afya tele, zitue kwako we mama,

Ninakupenda milele, sikuchukii daima,

Mazuri yakutawale, na upate mwisho mwema,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Leo nimeketi chini, kukutungia shairi,

Macho kwako hayaoni, isipokuwa ni kheri,

Haunikifu moyoni, kila siku u mzuri,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Mepita nyingi dahari, sikuwahi kutokea,

Japo ni ya mola siri, kuingia kwenye dunia,

Kwako we nikadhihiri, tumboni ukanilea,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Mahaba ya kila hali, mama ulinonyeshea,

Nikilia we hulali, shida wataka kujua,

Nisipokula hauli, na mengine wayajua,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Mukanikuza kwa tabu, sana nikawasumbua,

Wala hamkujaribu, mbali kunitupilia,

Sasa napata majibu, thamani nawapatia,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Mama ulinifundisha, pale nilipokosea,

Hukutaka kunichosha, mi nilipojichokea,

Menifundisha maisha, njia nisijepotea,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Wewe kwangu ndiye dira, mana umeniongoza,

Na kama nikikukera, usisite kunijuza,

Nakuombea akhera, akuridhie muweza,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Beti niandike kumi, mia elfu malaki,

Kwangu ni kama kichomi, pumzi hazivutiki,

Sifa zako hazikomi, tena hazina breki,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Wasijepumbazwa watu, wazazi kuwadharau,

Wakome wasithubutu, hata kwa uangalau,

Tuwavesheni viatu, jama tusiwasahau,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Kwa upendo na bashasha, ninajivunia mama,

Na hapa ndo nakatisha, mishororo kuisema,

Du’a kwako nazidisha, ulipo uwe salama,

Nakuita jina mama, kwa upendo na bashasha.

Liwafikie akina mama wote ulimwenguni

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *