(Picha kwa hisani ya Dreamstime.com)
{Na Abdul Shaban}
Nakumbuka siku hiyo, niliketi kitandani,
Alikuja mbiyombiyo, akalala kifuani,
Akiwa mwenye kiliyo, kama yuko msibani,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Kabla kumuuliza, tatizo ni kitu gani,
Ambacho kinamliza, akatoka furahani,
Akanambia sikiza, “ewe wangu wa hubani”
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Na mimi sikupuuza, kulifanyia utani,
Sauti nikapunguza, ya redio pale ndani,
Akaanza kunijuza, ili kunitoa dhani,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Kwa sauti ya kuimba, kama chiriku mbugani,
Ndipo akaanza amba, kimtiacho shidani,
Kuwa eti! Ana mimba, ni yangu si ya fulani,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Sikusubiri apoe, ama afike mwishoni,
Ikabidi niyatoe, niliyonayo moyoni,
Nikaanza na mayoe, yalonijaa pomoni,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
“Nyonda wangu taratibu, sikiza yangu maoni,
Japo jambo la aibu, mimba isiyo ndoani,
Kulea ninawajibu, usiwe mwenye sononi”
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Kwangu ikawa aula, sote tukiwa rahani,
Nikazidi saka hela, viwe havikosekani,
Vizurizuri vyakula, matunda pale nyumbani,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Ikakatika miezi, kwa rehema za Manani,
Nikiyatoa malezi, mzuri yenye thamani,
Akabariki Menyezi, kujifungua mwendani,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Huku nikiwa na hamu, nikawasili gangoni,
Mtoto nimfahamu, aliyetoka tumboni,
Sikuamini dawamu, nilichoona machooni,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Ayi! Nilipata tabu, sijawahi maishaini,
Nikaiona ajabu, mbaya isiyo mfani,
Ati! Napewa mwarabu, na mie hatufanani,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.
Tama naachia nibu, kuongeza sitamani,
Nyonda hana la kujibu, anaomba samahani,
Kwa haya yalonisibu, siwezi kutamakani,
Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.