Involvement

Umaskini tuuangamize au tuupunguze

Untitled
PHOTO COURTESY: ARON MTURI

Ni wangapi wamekuwa wakipoteza wapendwa wao kila mwaka kwa majanga yasiyoeleweka? Tume­kuwa tukijaribu juu chini kutafuta suluhisho, huku tukiambiwa kuwa kuna madaktari ambao hukesha wakitafuta dawa za kati ya magonjwa makuu yanayoangamiza binadamu. Kufikia sasa, bado watu wanatamani kupata suluhisho la jinsi watakavyopata dawa za magonjwa sugu kama vile UKIMWI…lakini la kushangaza ni kuwa hata ugonjwa wa Malaria unaweza kuti­bika, lakini kila siku, takriban watoto ELFU TATU wanaangamia. Ninavyofikiria ni kuwa, tumekuwa watu wanaojishughulisha na mengi hadi tunasahau madogo ambayo tunaweza kuyaondoa kwa haraka.

Katika Jamii, vijana wana mengi am­bayo wanaweza kuyafanya ili kushughulikia hili tatizo la umaskini, lakini tuseme ukweli, TUMEZEMBEA! Nilifurahishwa sana na jumbe niliyoipata kutoka kwa vijana kadhaa wa chuo kikuu cha Daystar ambayo ilikuwa hivi, “Tumekualika katika mkutano wa vijana, am­bapo tutakuwa tukiongea kuhusu jinsi sisi kama vijana tunaweza kuangamiza umaskini.”

Singetaka kukuelezeeni jinsi nilivyofika mkutanoni…nilifika mapema, na si uongo, nilitabasamu tangu hadi mwisho. Mkutano wenyewe uliongozwa na Bwana mmoja, Dan Orero, kwa kusema kuwa angependa kila mtu atoe maoni yake. Kivumbi kikaanza! Kwanza, Bwana mmoja aliamka na kusema kuwa kul­ingana na utafiti wa wataalam, imesemekana kuwa si rahisi KUUANGAMIZA umaskini. Tunaloweza kufanya ni KUUPUNGUZA… Kimya! Orero naye hakusema kitu, aliandika tu.

Zaidi ya hayo, aliuliza kama tunapaswa kui­lalamikia serikali kuhusu kiwango cha juhudi za kuupunguza umaskini. Hili lilimfanya Bwana mmoja kusema kuwa hatupaswi kuitupia seri­kali lawama, kwani haiwezi kufanya kazi bila kushirikiana na wananchi. Kisha, mwengine aliongeza kuwa tunazo rasilimali za kutosha na pia uwezo chungu nzima, ambao tumekuwa tukiupata tangu shule ya msingi, na kuna njia ambazo tunaweza kuzitumia ili kuupunguza umaskini katika jamii.

Karen, mmoja kati ya wengi waliokuwepo alisema kuwa wazazi wana jukumu kubwa sana katika kuhakikisha kuwa watoto wao watakuwa katika mstari wa mbele katika vita vya kupun­guza umaskini. Ili wazo hili lilete maana, Wa­zazi wana jukumu la kuwaunga mkono watoto wao katika lolote wanalotaka kufanya maisha­ni. Aliongeza kuwa watu wengi wamepata sha­hada, na wamekaa miaka kadhaa bila kazi kwa­sababu walichokifanya chuo kikuu hakiendani kamwe, na kilichokuwepo myoyoni mwao.

Hakuna aliyenifurahisha kama bwana mmoja, Gordon Odhiambo, aliyeongea kwa lugha ya kiingereza, “let us not come to school to GET JOBS, but to GIVE BACK TO THE COMMUNITY.” Ijapokuwa mimi si gwiji wa lugha ya kiingereza, nilimwelewa na kupasua kicheko. Watu walinishangaa kwa kudhani kuwa alikuwa ameongea upuzi mtupu, bali nilicheka kwani alikuwa ameigonga akili yan­gu kwa maneno ya busara ambayo nilikuwa nimeyatamani kwa muda mrefu.

Singependa kukueleza mengi, natumai umenielewa, lakini nitakuacha na swali amba­lo wengi wamekuwa wakijiuliza. Je, unafikiri kuwa umaskini unaweza kuangamizwa kabisa, au kupunguzwa tu?

By: Aron Mturi

(aronmmtunji@daystar.ac.ke)

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top