Involvement

TUMBIRI BWALONI

Na Mariita Joshua Ongoro

Nimefika kwenye bwalo, nipo foleni nawaona wanachuo kila mtu kashika hamsini zake. Nina mkoba wangu wa ngozi umening’inia begani na kila ninapotembea, mkoba nao unacheza densi ya shwii shwaa. Mwanangu nakumbuka kipindi kile nilikuwa shule ya msingi kijijini Gusii; Mabonde na milima, nilishuka na kupanda nikiwa na kijikoba cheusi chenye mkanda wa mchungwa. Unaelewa jinsi mvua ikianza kunya, hasa pale kijijini, hamna pa kujikinga maana migomba ya ndizi kila sehemu. Itakubidi ukurupuke mbio huku mkoba nao unakucharaza makofi kwenye vilima vya mwili – yaani makalio. Kaptura nayo ina vijisehemu vya kuingizia hewa kwa jinsi ilivyoraruka na kuchakaa, utadhani sehemu ile ya nyuma ina macho. Ukishafika nyumbani baada ya kukurupuka ja Nyantika Maiyoro, mkimbiaji shupavu wa Gusii siku za nyuma, utadhani madaftari kahariwa kule nyuma kumbe unyevunyevu na harufu ya jasho nzito.

Safari hii nimeepuka kuvaa kaptura ya aina yoyote na mkoba nimehakiki si wa mchungwa. Ingawaje ni mweusi, sasa ni wa ngozi, si wa nyuzi wala kitenge. Zamu yangu ya kuhudumiwa inatimia. “Nipe chai kwa maandazi halafu unitilie kayai kamoja.” Ninatamka bila ya kujali sarufi. Mbali na udunisho wa ‘kayai kamoja’ Inanikumbusha kuwa, ukienda Mwanza, basi utajutia kutohudumiwa unaposema ‘nipe’ kwani unamiliki wewe bidhaa hiyo? Tusiseme mengi maana hata salamu huja mwanzo. Je, Pwani yetu ya Kenya, maadili yamedumishwa ama vijana wameroga ufanisi huu kwa lugha za mitaani kama Shembeteng’ ya Jeshijinga? Kwanza hata kuwasikia leo imekuwa siwapati. Jamani nijibuni; Waliendapi Jeshijinga?

Taratibu natembea nikikokota miguu kana kwamba nipo mwezini ili nisilambe sakafu kwa pupa zangu. Naangaza macho yangu kuelekea meza iliyo pembeni mwa mlango wa kuvukia kwenda sehemu ya pili ya bwalo hili. Natabasamu japo mwonekano huu utadhani ninalia ndo maana hata nikaambiwa eti sura yangu mimi inaweza kuwachekesha wagonjwa hospitalini wakavunja mbavu hadi kupona kwa jinsi ilivyojaa makunyanzi. Basi ninapunguza tabasamu hilo la kutisha ninapokumbuka maneno ya abu. Ninachongea mezani na kuchukua uma. Cha kushangaza ni kwamba sikufahamu kuwa baada ya kumiminiwa chai pale bwaloni, ni jukumu langu kujitilia sukari. Mimi naye ninaenda zangu mezani na ninaonja ile chai, Lo! “Mbona hawatii sukari bwanaaa? Hii chai bubu sasa…” Ninajinung’unikia kwa tafsiri ya mama- bubu ni kinywaji kisichokuwa na sukari kwenye lugha ya kisiri ya Gusii. Muda nao unakwenda sana. Siwezi kurudi ili nitie sukari maana hata nishazoe mimi. “Kwanza sukari ni sumu mwilini, ni vizuri kunywa ya namna hii maana ni afya hii.” Ninajishawishi.

Punde tu nikiwa mjadalani, nasikia purukushani, viti vinasongasonga ovyoovyo. Ala! Hamna mtu bwaloni hasa upande huu wa chini. “Basi nini?” Ninakodoa macho upande wa kushoto nawaona tumbiri, mama yangu! Hivi, nitakunywa chai kweli ama nimewanunulia hawa wapumbavu? Tunaangaliana maana kila mmoja yuko chonjo. Kidogo tumbiri anaruka mezani. Mimi ni mwanaume siwezi kuchezewa shere hii. Ninanyanyua mkono na kuuchezesha kuelekea kwake yule mshenzi, kana kwamba ni nyoka anayeinda na huku usoni nimetia makunyanzi tishti.

Ni kweli tumbili naye alihofia maisha yake mafupi ila hakuchoka. “Mimi kwanza ni mwanamme na tumbiri huwaogopa sana wanaume. Si nawaona jinsi wanavyowaangaisha wanadada chuoni zaidi ya wanaume.” Nikajitia nguvu. Upo wakati nilikuwa nikitokea zangu maabara ya kompyuta kule epada yaani EPD, kwa umbali nikawaona wanadada wamekongamana sehemu moja kijia-panda cha SBE. Nikawa sina habari ya lile kundi lililozubaa. Basi kwa mpito wangu nikiwa nimetangulia nawasikia nyuma yangu wamefuata. Ninashangaa. Kumbe mwanangu, wasichana wale walikuwa hawana mtu wa kuwavusha kwenye bahari shamu ya tumbiri waliofurika nje ya shule ya sheria. Basi nikawa Musa niongozaye huku nyuma yangu Waisraeli wamenifuata wakielekea ‘Kanani.’

Kwenye idara ya Saikolojia, ipo nadharia inayoitwa; Uhamisho wa elimu ambayo kwa kimombo tunaita ‘transfer of knowledge’ ambayo hufundisha kwamba, mtu husuluhisha tatizo kutokana na kusoma yaliyotendeka nyumaye. Mimi kama mwanasaikolojia nilikumbuka kuwa hawa tumbiri huwaogopa wanaume. Basi, mimi ni nani? Lazima niwatishe hawa washenzi. Lakini haikuwa rahisi. Mezani ninaamua kupapia maandazi yale ili angalau nisitoke bilashi. Sasa siwezi kutumia uma kula kwa ustaarabu ila mikono. Upande mwingine namsikia tumbiri mvunguni mwa meza anatapatapa kwa kucha zake. Ninaanza kurusha mateke, “Mniache bwana.” Ila ninapomshtua basi anaruka mezani. Kwa ufundi huu wa kula ninasafisha sahani FYU na ninabakia na yai. Chai sijanywa. Ninachukua uma na kuanza kutoa maganda lakini siwezi maana nimekazwa sana. Naitumia mikono tena. Ninatafuna kipapachipapachi huku nikiangazaangaza macho utadhani naiba kula. “Basi mnyweni hiyo chai ‘bubu’ maana hata haina faida.” Ninakejeli nikijipangusa midomo kwa hanchifu yangu ya zambarau na madoadoa ya samawati. Nimeshinda vita maana hata chai hawakunywa.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top