Na: Wangu Kanuri
kanuriwangu@gmail.com
TOA maelezo yako kuhusu mchezo wa raga
Raga ni mchezo ambao unahitaji nguvu haswa kwenye misuli. Mchezo huu umegawanywa katika makundi mawili makuu; ya wachezaji saba na ya wachezaji kumi na tano. Kundi hili la wachezaji saba hujulikana vyema kama rugby 7s ilhali hilo la wachezaji kumi na tano hujulikana kama rugby 15s. Vikundi hivi ndivyo vimepewa kipaumbele nchini ila kuna vingine.
TUELEZE kwa ufupi kukuhusu
Slyvester Miheso, ni mwanafunzi wa shahada ya Udhibitishaji wa Rasilimali za Nchi katika chuo kikuu cha Daystar. Anapenda kusikiza muziki, kufanya mazoezi na kutizama filamu. Isitoshe, mimi ni mchezaji wa kawaida katika timu ya Falcons ambayo ni timu ya raga katika chuo kikuu cha Daystar.
NINI kilikuchochea kuupenda mchezo huu wa raga?
Nilipojiunga na shule ya upili ya Mtakatifu Inyasi ndipo ari yangu ya kupenda mchezo wa raga ilianza. Nilijiunga na timu ya raga nikiwa kidato cha kwanza japo shingo upande kwa kuogopa kuumizwa. Baada ya kujiunga na mchezo huo nilijua sheria na masharti zinazomkinga mtu wakati wa kumenyana na hofu yangu ikapungua.
NI mchezaji yupi katika raga hukuvutia? Kwa nini?
Mchezaji ninayemuenzi anachezea timu ya na Mwamba anafahamika kama Collins Injera. Mchezaji huyu ana bidii na anapenda kuwapa mwelekeo wachezaji chipukizi ili waweze kubobea kama yeye. Isitoshe, Collins amejivunia taji nyingi katika ligi za Uingereza kwa kufunga mabao mengi.
MCHEZO HUU umekuvunia tija ipi?
Mchezo huu umeniwezesha kufadhiliwa kimasomo katika ya shule ya upili na ya chuo kikuu. Hali kadhalika, nimejivunia taji la mchezaji bora na pia mchezaji aliyefunga mabao mengi upande wa Division 2. Nimeweza kuzuru nchi ya Uganda na Rwanda na miji ya Kisumu, Kakamega, Nairobi, Meru, Nanyuki na Nakuru.
UNAWASHAURI vipi wachezaji chipukizi?
Wasififishe talanta zao kwani ni zawadi kutoka Maulana. Pili, wafanye bidii wakati wa mazoezi huku wakiamini wao ni wachezaji bora kwani jambo huanzia kwa kukata shauri akilini. Tatu, wasikate tamaa hata wakishindwa kwani kufeli si kujaribu bali kutojaribu.