Involvement

NYAMA NI ILE ILE

{Picha kwa hisani ya Organic Authority}

 

Na Abdul Shaban

 

Mabucha utabadili, nyama ni ile ile
Wa kizungu na swahili, uitakayo uile
Kwa chumvi na pilipili, hata uunge tungule
Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

Nyama zote mabuchani, zatoka machinjioni
Hizo ndo zenye idhini, zipikwe kwako nyumbani
Umbile lisikukhini, minofu ilosheheni
Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

Uzuri wa kula wali, usiule kwa tembele
Hata ikiwa ugali, chuzi si kipau mbele
Njaa ikikukong’oli, siyo chochote ukile
Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

Iwe nyama ya mnofu, ama ile ya mfupa
Usikukhini upofu, kutotaka toka kapa
Kuparamia nyamafu, dhana kwamba ndiyo supa
Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

Nyama ilofungashoni, hiyo ndiyo yakufaa
Uile kama pudini, wima ima ukikaa
Alokuridhi #Manani, halali kwako asaa
Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

Uzuri wa kula nyama, ukosheke fuadini
Sihadaike mtima, viso kwako mkononi
Kutwa ukazisakama, eti uwe furahani
Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

Fumbo hili ni jepesi, ulifumbue hadhira
Sijafanya udamisi, ni insafu nimechora
Wala si utusitusi, ila yangu tabasura
Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top