{Picha kwa hisani MyBroadBand}
Na Dennis Mungai
Raundi ya nne ya mechi Ligi kuu nchini Uingereza imekamilika wikendi hii siku ya Jumapili, mechi ya mwisho ikiwa baina ya Arsenal dhidi ya Manchester United. Mechi yenyewe ilikua ya kusisimua, The Gunners wakipata ushindi wa mabao tatu kwa moja. Declan Rice alifunga bao lake la kwanza kama mchezaji wa Arsenal kisha Gabriel Jesus kufunga la tatu na kuhakikisha ushindi wao. Bao la United lilifungwa na Marcus Rashford kisha Martin Odegaard kusawazisha dakika moja baadaye. Vijana wa Erik Ten Hag sasa wapo katika nafasi ya kumi na moja wakiwa na alama sita huku Arsenal wakiwa na alama kumi.
Siku ya Jumamosi ilishuhudia wachezaji watatu wakifunga mabao matatu kila moja, ama kwa Kimombo “hat-trick”. Evan Ferguson wa Brighton alifunga mabao matatu kusaidia timu yake kupiga Newcastle 3-1. Erling Haaland alifunga mabao matatu pia na kuzalisha lingine huku vijana wa Pep wakigaragaza Fulham 5-1. Mabao mengine yalifungwa na Nathan Ake na Julian Alvarez. Spurs walishinda Burnley 5-2, Son Heung-Min akicheka na wavu mara tatu huku Romero na James Maddison wakiongezea vijana wa Vincent Kompany masaibu baada ya kupandishwa daraja msimu huu.
Jurgen Klopp alipata ushindi wa 3-0 katika mechi yake ya mia tatu kama mkufunzi wa Liverpool. Szoboszlai na Salah walifungia Reds huku difenda wa Aston Villa Matty Cash akijifunga. Crystal Palace walipata ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Wolves nayo Chelsea walilazwa 1-0 na Nottingham Forest.
Siku ya Ijumaa West Ham walishinda Luton Town mabao mawili kwa moja, Jarrod Bowen akiendeleza msururu wake wa kufunga mabao msimu huu. Brentford na Bournemouth walitoka sare ya mabao mawili nayo mechi ya Sheffield United na Everton kumalizika kwa matokeo sawia. Ligi itachukua mapumziko ya mechi za kitaifa za kirafiki na itaendelea tarehe kumi na sita mwezi huu.