Involvement

Matokeo na Matukio Ligi Kuu Nchini Uingereza

{Picha kwa hisani ya Bekaboy}

 

Na Dennis Mungai

Raundi ya pili za mechi ligi kuu nchini Uingereza ilikamilika jana usiku wakati Arsenal walichuana na Crystal Palace ugani Selhurst Park. Vijana wa Mikel Arteta walipata ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya mahasimu wao wa jadi kupitia penalti iliyofungwa na Martin Odegaard. Beki wa Arsenal Takehiro Tomiyasu alionyeshwa kadi nyekundu lakini the Gunners walishikilia bao lao na kutoka na alama tatu.

Katika mechi nyingine, Brighton walipata ushindi sawia na ule wa wikendi uliopita kwa kuigaragaza Wolves 4-1  Siku ya Jumamosi. Mabao yao yakifungwa na Solly March, Kaoru Mitoma na Pervis Estupinan. The Seagulls wanaongoza jedwali kwa alama sita na wanaonekana kuwa wakali zaidi licha ya kuuza Alexis Mac Allister na Moises Caicedo. Newcastle United walishindwa na Man City 1-0, bao hilo likifungwa na Julian Alvarez.

Manchester United walipoteza mechi yao dhidi ya Spurs walipopigwa mabao mawili kwa bila. Mabao ya Spurs yalifungwa na Pape Sarr na mlinzi wa Red Devils Lisandro Martinez alijifunga. Aston Villa waliwaduwaza Everton 4-0 huku mshambuliaji Dominic Calvert Lewin wa Everton akipata jeraha nyingine la uso. Brentford waliendelea kuwashangaza wengi kwa kuipiga Fulham mabao matatu bila jibu na sasa wana alamu sita na kuchukua nafasi ya pili  katika jedwali.

Mohamed Salah alimpiku Steven Gerrard katika orodha ya wafungaji bora Liverpool kwa kufunga bao katika ushindi wao wa mabao tatu kwa moja dhidi ya Bournemouth. Luis Diaz na Diogo Jota pia walifungia the Reds. Bao la Bournemouth lilifungwa na Antoine Semenyo.

Siku ya Ijumaa Nottingham Forest ilipata ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Sheffield United. Mechi ilikaribia kukamilika ikiwa sare lakini mshambuliaji Chris Wood aliingia uwanjani na kutia kimiani bao la ushindi. Raundi ya tatu itaanza siku ya Ijumaa wakati Chelsea itaialika Luton Town ugani Stamford Bridge. Vijana wa Mauricio Pochettino wanatafuta ushindi wao wa kwanza baada ya kupigwa 3-1 na West Ham siku ya Jumapili.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top