Involvement

LIGI KUU NCHINI UINGEREZA

Mlinzi wa Manchester United Raphael Varane asherekea bao la pekee katika mechi dhidi ya Wolves siku ya Jumatatu.

{Picha kwa hisani ya Premier League}

 

Na Dennis Mungai

 

Jana usiku Manchester United waliialika Wolverhampton Wanderers ugani Old Trafford kwa mechi ya ufunguzi baina ya timu hizo katika msimu mpya wa 2023/24. Wachezaji wapya wa United Andre Onana na Mason Mount walikua katika kikosi cha kwanza. Mshambuliaji wao mpya  Rasmus Hojlund alipata jeraha kabla ya msimu kuanza hivyo basi alikua nje ya kikosi. Wolves walipata upenyo katika ulinzi wa United na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kupitia wachezaji Matheus Cunha na Pedro Neto lakini hawakupata bao.

Hatimaye katika kipindi cha pili bao la pekee lilifungwa na mlinzi wa United Raphael Varane baada ya kupewa pasi na Aaron Wan Bissaka. Vijana wa Erik Ten Hag watahisi kutoka na ushindi huo ulikua kibahati kwani Wolves walicheza mchezo bora zaidi katika mechi hiyo. Ushindi huo unakamilisha mechi za ufunguzi katika ligi hiyo.

Newcastle wanaongoza jedwali kwa alama tatu baada ya kuivuruga Aston Villa 5-1 siku ya Jumamosi, huku Brighton wakichukua nafasi ya pili baada ya kuilaza Luton Town mabao manne kwa moja. Arsenal walianza msimu kwa kuipiga Nottingham Forest mabao mawili kwa moja. Mabingwa watetezi Man City walifungua msimu kwa kuishinda Burnley 3-0. Mfungaji bora Erling Haaland aliendeleza alipoachia msimu uliopita kwa kutia kimiani mabao mawili. Fulham na Crystal Palace walipata ushindi sawa wa bao moja kwa bila dhidi ya Everton na Sheffield United.

Siku ya Jumapili mechi ya Brentford dhidi ya Spurs ilitoka sare ya mabao mawili huku vijana wa Ange Postecoglou wakianza maisha bila mshambuliaji matata Harry Kane. Mabao ya Spurs yalifungwa na Cristian Romero na Emerson Royal. Pochettino alishika usukani kama kocha wa Chelsea na mechi yake ya kwanza dhidi ya Liverpool ilitoka sare ya bao moja. Luis Diaz alifungia the Reds bao la kwanza kisha mlinzi  mpya wa Chelsea Axel Disasi kusawazishia the Blues dakika chache baadaye.

Ligi hiyo itaendelea wikendi hii, mechi ya kwanza ikiwa siku ya Ijumaa wakati Nottingham Forest itaialika Sheffield United ugani City Ground.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top