Involvement

Hongera Septemba

Na Mariita,

Muhula wa Septemba umejawa na matukio mbalimbali ikiwemo michezo ya Falcon, burudani, wiki ya maonyesho ya mila na desturi za Kiafrika, biashara, utandawazi, mkutano wa kukuza mambo ya nje na mahusiano ya kimataifa vilevile kuweka msingi wa ujenzi wa maskani ya wanachuo.

Hatua hii muhimu ya kulishughulikia suala la maskani, imeibua hisia chanya kwani Naibu Chansela Prof. Ayiro na bodi ya chuo hiki, amefanikisha mchakato wa mradi huu kwa upesi. Kwingineko, mradi wa ujenzi wa Mama Musau- Shule ya Sheria, unazidi kunoga kwani ukitembea kwenye sehemu ya tukio la ufundi, utashibishwa na mizani ya waashi ilivyoimara. Ni wazi kwamba Imani ya wengi sasa imetiwa kwenye kiambo.

Aidha, kuna hamu kubwa ya kutaka chuo hiki kuangazia mradi ambao wengi watauita ‘MAMA YAO’ kwani kiuhalisia, bila pingamizi na kwa ushawishi mkubwa; Chuo Cha Dayastar kinafahamika nchini na ukandani kama Chuo Cha Mawasiliano. Uvumi wa sifa zake ni kama mawimbi baharini, kuenea kwa ubora huu kumetikisa mashariki na kati. Kiukweli, shule ya mawasiliano imepeperusha bendera na kuwa kama kitambulisho kamili cha Chuo Cha Daystar.

Kituo chetu cha Redio Ya Shine, mitabendi 99.9 kingali kinafanyiwa ukarabati na hayo ni maendeleo kwenye sekta ya mawasiliano. Zaidi, ingelikuwa bora mno ikiwa kituo cha televisheni, ambacho sio tu kwa kuleta programu mbalimbali zihusianazo na habari, burudani, kupeperusha ibada chuoni na matukio ya ukuaji, kingelipata sehemu mwafaka ambayo ni jengo la shule ya mawasiliano ili kufufua uwajibikaji kwa kutoa motisha na kuwapa kipaumbele wenye talanta mbalimbali.

Safari ya maendeleo italazimu kila mmoja kujibidiisha ili kudumisha sura ya Chuo na maadili kama mojawapo ya changizo katika kuimarisha ubora wa masomo na uongozi tabithi. Muhula huu wa Septemba unazidi kufunua vyungu vya mabadiliko na vilevile kupekua kurasa za maendeleo mahali mahali.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top