Involvement

HEKAHEKA ZA MUHULA WA SEPTEMBA

Na Mariita Joshua Ongoro

Ni kweli kwamba mihula ya masomo hapa chuoni huwa na mambo yanayochipuka mwanzoni, kati na hata mwishoni. Muhula ukianza kawaida kuna kule kung’ang’ana na hali ya ulipaji karo, usajili wa masomo na mahudhurio ya mara kwa mara. Zaidi, hamna jambo linalobubujisha msongo wa mawazo kama vile kukosa chumba cha kupanga. Je, ni wangapi huzurura kotekote, mapana na marefu, kujaribisha nasibu ya kupanga angalau hata mabatini? Wakati mwingine huambulia patupu kwa kusononeshwa na kauli za wasimamizi wa vyumba vya kupanga, “Hamna chumba labda ujaribishe huko Portland.” Tabu. “ Ama kama hutojali, kunacho chumba pembeni kuleee… hakina umeme ila baadhi ya wenzenu wameshawahi kuishi siku za nyumba hali hii ilipojitokeza.” Utamsikia akiongeza kwa kutojali kana kwamba ni jeuri.

Mbanano wa wanachuo nje ya shule imeleta hali chanya na pia hasi. Vyumba vya kupanga kila sehemu vimebeba mamia ya wanachuo na ni dhahiri kwamba wamiliki wa vyumba hivyo, hawajajutia ujenzi wao japo uliwagharimu kiasi kikubwa cha fedha. Kwa upande mwingine, uhitaji wa upangaji umeibua mijadala na hisia tofautitofauti kuhusu ongezo la kodi. Vyumba ni vile vile, hali ni ile ile, wanafunzi ni wale wale, maji ni yale yale tena ya chumvi; itakuwaje kuongeza kodi hata muda hamna vyumba vya kupanga? Sarakasi hii, pengine inawafaidi pakubwa wasimamizi hata kupita wamiliki halisi.

Uhalisia wa elimu ya chuo inafafanuliwa kivipi? Je, kuna namna inayoweza kujitokeza ili iwe suluhisho kwa misukosuko na mawimbi ya jinsi hii? Cha kusikitisha ni kwamba, jinsi ujio wa wanachuo unazidi kunoga, basi hali hii inazidi kuyumbisha matamanio. Ingawaje kuna mahafali wa kila mwaka, wanaoingia huzidi mtoko. Sintofahamu inayopeperusha bendera miongoni mwa wanachuo ni kwamba chuo hiki, kwa jinsi kinavyofahamika kwa sifa zake, je, haingekuwa dhahiri kuwekeza katika miradi inayowanufaisha wanafunzi maana hawa ndio walengwa wakuu?

Hatuwezi kulifumbia macho suala la Naibu Chansela, Prof. Ayiro kuchakatua miradi ya maendeleo kila baada ya muhula ama tuseme kila siku. Ni wazi bila pingamizi kuwa kati ya wazalendo na wachapakazi wa kweli, basi Profesa Ayiro amevikwa taji kwani ni mmoja wao na pengine kiongozi wao. Lakini mojawapo ya wasilisho la ombi kuu ambalo lingehitaji uchambuzi ni hili: Ujengaji wa vyumba vya malazi kwenye ardhi ya chuo hiki.

Umuhimu wa ujenzi wa vyumba hivi ni pamoja na kodi inayoweza kugharamiwa na wanachuo hata wa kiwango cha chini. Ukengeufu uliopo kwenye mazingira ya nje ya shule ni pamoja na ukosefu wa maji, maji yasiyo safi kwa hali ya kutotibiwa mfano kwa njia ya klorini. Ukuaji wa chuo hiki kunategemewa na vizazi kwa sababu kutawafaidi waliomo na wasiokuwemo. Hivi sasa wanachuo wanazidi kukumbwa na hali ya kumudu maisha na pia utekelezaji wa majukumu yao kama vile kufika chuoni kwa wakati, kutimiza maono na lengo la elimu. Ladha ya kufanikisha vipengele vyote muhimu itatiwa kwa kulainishwa kwa masuala tata kama haya ya upungufu wa vyumba vya kupanga. Hekaheka za Septemba zahitaji hali kutengemaa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top