Skip to content

Involvement

Home » KAYOLE INAOMBOLEZA

KAYOLE INAOMBOLEZA

Na Chelangat Caren,

Jioni ya Mei 18, 2026, maneno hayo yalirudi kwa wengi wa Nairobi kama mshale. Siku hiyo, sauti ya Rachael Wandeto ilinyamaza milele. Mwanamuziki wa injili, mama, dada, na sauti iliyokuwa ikisikika kanisani na mitandaoni, alifariki katika shambulio la moto linaloshukiwa kuwa la kisiasa;alikua na miaka 31 tu.

Rachael hakuzaliwa maarufu. Alikulia Kayole, akipanda daladala asubuhi na mapema kwenda mazoezi ya kwaya Buru Buru. Marafiki zake wanasema alikuwa wa kwanza kufika na wa mwisho kuondoka. “Kama hukuimba kwa moyo, usiimbe kabisa,” alikuwa akiwaambia watoto wa Sunday School walipomzunguka baada ya ibada.

Wimbo wake wa kwanza, “Nitashinda”, ulivuma mwaka 2023. Sio kwa sababu ulikuwa na beat nzito, bali kwa sababu ulikuwa na ukweli. Rachael aliimba kuhusu kufeli, kupona, na kuamka tena. Vijana wengi waliuona kama wimbo wao wa maisha.

YouTube yake ilifikia watazamaji 200,000 kwa muda wa miezi sita. Alikuwa anakaribia kutoa album yake ya pili. Ilitokea Kayole, nyumbani kwake. Majirani wanasema waliona watu wawili wakishuka kwenye pikipiki muda mfupi kabla ya moto kuwaka. Ndani, Rachael alikuwa peke yake. Mumewe alikuwa kazini Mombasa, watoto wawili kwa shangazi.

Moto ulizima kabla ya kufika vyumba vya jirani, lakini chumba cha Rachael kiliteketea. Polisi wanasema uchunguzi unaendelea, lakini tayari kuna uvumi kuwa ilikuwa kulipiza kisasi kisiasa. Rachael hivi karibuni alikuwa amechapisha wimbo unaokosoa unyanyasaji wa kisiasa dhidi ya vijana.

“Kama ni siasa ilimuuwa, basi tumepoteza zaidi ya mwanamuziki,” aliandika mmoja wa mashabiki zake X. “Tumepoteza dhamiri. “Habari ya kifo chake ilisambaa haraka. Kanisa la PCEA Kayole lilijaa siku iliyofuatia. Vijana walibeba mabango yakiandika “Rachael, Uliimba Kwa Sisi”

Mike Sonko alifika na maua meupe. Eric Omondi, ambaye siku moja kabla alikuwa mtaani na jerricans tupu, alisimama nje ya nyumba yake na kusema, “Hii si siasa tena. Hii ni maisha ya mtu.”

Mitandaoni, hashtag #JusticeForRachael ilipanda hadi nafasi ya pili nchini. Wasanii kama Mercy Masika na Guardian Angel walipakia video wakilia na kuimba mistari yake.Lakini kati ya machozi yote, kitu kimoja kilirudiwa: Rachael alikuwa wa watu wa kawaida. Hakuwahi kusahau Kayole. Alikuwa anafadhili masomo ya watoto watatu wa yatima. Alikuwa ananunua unga kwa wajane wa kanisani kila mwisho wa mwezi.

Mazishi yatafanyika Jumamosi nyumbani kwao Kisii. Lakini tayari wengi wanasema Rachael hatazikwa kweli. Kila wakati kijana anapopata nguvu ya kusimama baada ya kuanguka, anaimba “Nitashinda”. Kila wakati mama anaposhindwa kulipia nauli lakini bado anaamini kesho itakuwa njema, anasikia sauti ya Rachael.

Siasa inaweza kuchoma nyumba. Risasi inaweza kunyamaza mdomo. Lakini wimbo unaoingia moyoni hauwezi kufa.Rachael Wandeto alikuja kimya, akaimba kwa nguvu, akaondoka ghafla. Sasa ni jukumu letu kuhakikisha wimbo wake hauzimi na yeye.

Kwa sababu kama alisema mwenyewe katika wimbo wake wa mwisho kabla ya kufa:  “Wakiuzima mshumaa wangu, nitawaka kama jua.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *